Thursday, August 13, 2009

Aina za viatu kwa kinababa


VIATU ni kati ya mavazi ambayo mara nyingi hayatiliwi maanani sana na wanaume, kama ilivyo kwa wanawake ingawa viatu vya wanaume ni aghali zaidi ya vile vya wanawake lakini je, wanaume hao wanaelewa kuwa uvaaji wa viatu huenda sambamba na mavazi yao na kuchangia waonekane watanashati?

Uchunguzi unaonyesha kuwa wanaume wengi hawatilii maanani suala la uvaaji wa viatu katika kukamilisha mavazi yao wengi wao wanadhani wanaweza kuvaa viatu vya aina na rangi yoyote wakatoka bila kujali nguo ulizovaa, shughuli wanayofanya wala hali ya hewa.

Watu wengi wanazingatia kununua tu nguo lakini si viatu. Katika hili wanaume ndio wanaonekana kuathiriwa zaidi na tabia hii, kwani mara nyingi wamekuwa wakionekana kutojali sana mitindo ya viatu.

Suala la kuwa na viatu vingi wao huona kama linamhusu zaidi mwanamke na si mwanaume. Mara nyingi huonekana kutilia mkazo masuala ya utanashati katika kutengeneza ndevu na nywele na nguo na kusahau kabisa kwenda na wakati katika mitindo ya viatu.Tena wapo ambao hawaoni tabu kuvaa viatu vya ofisini nyumbani au katika shughuli ambazo ni tofauti kabisa na mazingira ya ofisi.

Mfano, wanaume ambao ni askari utakuta ni kawaida kwao kuvaa viatu vyao vya ofisini katika sherehe au shughuli nyingine tofauti na zile za kiofisi na kusahau kuwa aina hizo za viatu vinatakiwa kuvaliwa kama sare ya kazini kwenye shughuli za shuluba.

Wataalam wa mambo ya mitindo wanashauri viatu kuvaliwa kulingana na shughuli iliyokusudiwa na wanaume wanatakiwa kuwa na viatu zaidi ya jozi nne, hii itasaidia sana kuwafanya waonekane watanashati na wenye kujua maana katika mitindo na fasheni kwa ujumla.

Kwa vazi la jeans
Suruali ya jeans huvaliwa na viatu vya rangi na aina tofauti tofauti ingawaje wataalamu wa mambo ya mitindo wanashauri kutokuvaa viatu vyenye rangi ya kuwaka sana kwani itapoteza maana.

Buti, raba, makubazi ni baadhi ya viatu vinavyoendana na jeans, hivyo ni jukumu la mvaaji kuoanisha vazi lake na shughuli anayoikusudia kufanya akiwa katika vazi hilo.

Na hakikisha viatu na jeans yako vinaendana na fulana au shati ulilovaa ili usionekane kichekesho katika tasnia ya mitindo.

Kwa nguo za kawaida
Mwanaume kama ilivyo kwa mwanamke huwa anakuwa na shuguli zake za kawaida ambazo si za kiofisi wala sherehe, hapa hulazimika kuvaa mavazi ya kawaida (casual wear).

Katika mavazi haya aina ya viatu inategemea na aina ya vazi hilo kama atakuwa amevaa pensi na fulana au kaptula na fulana unashauriwa kuvaa makubazi au hata raba na utakuwa na muonekano mzuri.

Ikiwa kama una safari fupi na upo katika vazi la pensi ndefu waweza kuvaa buti na ukaeleweka.

Kwa suruali ya kitambaa
Ikiwa utakuwa umevaa suruali ya kitambaa unashauriwa kuvaa viatu vinavyoendana na suruali hiyo mfano unaweza kuvaa kiatu cha ngozi cha kufuta, ili uonekane unayelewa mitindo unatakiwa kuhakikisha kuwa rangi ya viatu vyako inaendana na rangi ya mkanda au ya suruali yako.

Kwa kufanya hivyo utakuwa umeeleweka vizuri katika suala zima la mitindo na pia itakufanya uonekane wa kuvutia na kupendeza.


tips za uvaaji wa viatu kwa wanaume

*Jaribu kuchagua viatu vinavyoendana na suruali yako au vyenye rangi ya giza zaidi ya suruali yako.
*Unapofikiria viatu pia jaribu kufikiria kuhusu soksi hakikisha soksi zako ikiwa umevaa viatu vya kutumbukiza zinaendana na rangi za nguo ulizovaa, mfano haipendezi kuvaa viatu vyeupe na soksi nyekundu.
*Kama umevaa mkanda jitahidi rangi ya mkanda huo ifanane na viatu vyako.

*Hakikisha unakuwa na viatu na mkanda wa rangi nyeusi na vya rangi ya kahawia kwani vitu hivi kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya mitindo vinakubali aina nyingi za nguo. Hivyo inapendeza wanaume kuwa na vitu hivi.

*Ikiwa utavaa kaptula ya jeans au pensi tafadhali hakikisha unavaa na ‘sneakers’ au makubazi na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment