Thursday, August 13, 2009

Unazijua Kashda, au shemagh?
KASHDA ni aina ya kilemba ambacho kiasili kimekuwa kikivaliwa na watu wa nchi za kiarabu,wakijizungushia au kujifunga kichwani na wakati mwingine hadi maeneo ya usoni.
Kilemba hiki wakati mwingine hutumika kama vazi maalum kwa wanaume hasa wanajeshi wa nchi, hasa pale wanapokuwa katika shughuli zao kutokana na hali ya hewa hulazimika kuvaa vazi hili ili kujikinga na jua.
Katika nchi hizo hufahamika kama shemagh au Kefeyah. Hivi sasa kimekuwa katika chati za juu za mitindo kwa kutumiwa kama ‘scarf ‘inayotumika kuzungushiwa shingoni.
Tofauti na ilivyokuwa awali kitambaa hiki kwa sasa huvaliwa na wanawake na wanaume tena wakiwa katika mavazi mbalimbali na kuwafanya waonekane wenye kujua na kujali suala zima la ubunifu katika mitindo.
Katika kipindi cha hivi karibuni kitambaa hiki kimekuwa gumzo kwa wapenzi na wadau wa mitindo, na cha kufurahisha zaidi ni pale baadhi ya wasanii maarufu duniani walipoonekana wakiwa katika vazi hili kitendo kilichochangia kuhamasisha zaidi mtindo wake.
Kanye west mwanamuziki kutoka nchini Marekani ni miongoni mwa wasanii wakubwa walioonekana wakiwa katika vazi hili, ambapo mara baada ya kuonekana mtindo huu ulionekana kupokewa na watu wengi.
Nchini mbunifu wa mitindo Ally Remtullah amekuwa akitumia kitambaa hiki kama pambo lake kubwa ambapo mara kadhaa amekuwa akionekana akijitupia shingini hasa wakati akifanya utambulisho katika maonyesho yake.
Katika mtindo wa kisasa kitambaa hiki huvaliwa kwa kuzingishwa shingoni, au kutupiwa kichwani tofauti lakini huvaliwa katika mavazi tofauti tofauti na watu tofauti tofauti.
Namna ya kuvaa kashda.
Kwa kawaida kitambaa hiki huwa na pembe nne, kikiwa na rangi mboli pia ni huwa ni chepesi na zaidi huwa na urembo kuzunguka pande zote nne.
Kwa kawaida mvaaji hutakiwa kukikunja kitambaa hicho kwa kuchukua pembe moja kuilinganisha na nyingine ili kupata umbo la pembe tatu.
Baada ya hapo unaweza kukivaa katika mitindo mbalimbali kulingana na matakwa yako. Kwani unaweza kukitupia mgongoni huku pembe mbili zikitokea kwa mbele na kukifunga vizuri.
Pia unaweza kujitanda kichwani au wakati mwingine pia si vibaya ikiwa utajizungushia shingoni kwani bado utaonekana unakwenda na wakati.
Mtindo huu kwa kawaida unaendana na mavazi ya aina mbalimbali ingawaje umeonekana kupendeza zaidi katika vazi la jeans, ambapo mvaaji huvaa suruali ya jeans akichanganya na ‘top’ au fulana ya kisasa na hivyo kuonekana bomba zaidi.


Si hivyo tu baadhi ya wadau wa mitindo wamekuwa wakishauri mtindo huu kutokuvaliwa na nguo ndefu sana kwani zinakuwa hazileti maana iliyokusudiwa ambapo mvaaji huonekana kama amebeba mzigo.
Si hivyo tu mtindo huu hutumiwa kama pambo kwa ajili ya kuvaa katika nguo za kawaida (casual) hivyo si sahihi kabisa kuvaliwa katika maeneo ya kazi au kutumiwa na wanafunzi wakati wakiwa mashuleni.
Kwa upande wa viatu unaweza kuvaa na viatu mbalimbali kulingana na aina ya nguo ulizovaa , tofauti na vitambaa vingine kitambaa hiki kinaweza kuvaliwa katika vazi la ufukweni na bado kikaleta maana katika mitindo.

No comments:

Post a Comment