Tuesday, March 13, 2012
Tunic blouse
Katika ulimwengu wa mavazi, kuna mitindo mingi ambayo imekuwa ikishamiri na baadaye kupotea. Lakini kwa wakati huu vazi ambalo limeshamiri ni ‘TUNIC’ambalo lipo katika aina mbili, ambazo ni ‘tunic’ blauzi na magauni. Katika makala hii tutaangalia blauzi za tunic, ambazo kwa sasa zipo katika chati, sio tu hapa nchini bali duniani kwa ujumla.
Tofauti na nyingine aina hii ya blauzi huwa ni ndefu na inayoziba sehemu ya ‘hips’ na kuishia kwenye magoti. Pamoja na kuwakubali wanawake wengi, aina hii ya blauzi ni miongoni mwa mavazi mahsusi kwa watu wenye maumbo makubwa. Kwani kutokana na muundo wake huwapa nafasi wavaaji kuziba baadhi ya sehemu za maumbo yao hususan ‘hips’.
Si hivyo tu wakati mwingine tunic hupendeza zaidi pale zinapovaliwa na wajawazito kwani huwafanya wajisikie huru wakati wote. Aina hii ya blauzi, zimebuniwa katika nakshi mbalimbali zikiwamo za rangi moja.
Watumiaji wa vazi huusifia mtindo huu kutokana na sifa yake ya kuweza kuvaliwa katika matukio na wakati wowote.
Wakati mwingine hutumika kama vazi la kawaida. Lakini ikiwa mvaaji husika ataongeza baadhi ya mapambo huweza kulipa hadhi na zaidi na kuweza kuvaliwa hata kwenye mitoko mbalimbali.
Kwa upande wa hali ya hewa, aina hii ya blauzi ina sifa ya kuvaliwa katika misimu mbalimbali. Ikiwa utavaa wakati wa joto, unaweza kuvaa yenyewe kama ilivyo. Lakini ikiwa itavaliwa wakati wa baridi, unaweza kuvaa na blauzi nyingine kwa ndani hususani yenye mikono mirefu.
Ikiwa uko kwenye maeneo yenye baridi sana, si vibaya ikiwa utatumia ‘pull neck’. Kwa upande wa viatu, tunic huvaliwa na viatu vya aina mbalimbali kutegemea na mahali unapokwenda na shughuli unayokusudia kufanya. Ikiwa upo kwenye matembezi ya jioni unaweza ukavaa aina hii ya blauzi na leggings ama ‘skinny jeans’ na kutupia viatu aina ya makubadhi au ‘gladiators’.
Jambo la msingi, unalotakiwa kuzingatia, ni umbo lako na rangi ya blauzi hizo. Kama una umbo kubwa sana unashauriwa kutumia mavazi yenye rangi ya giza na ukiwa umbo dogo vaa yale yenye rangi za kuwaka. Hii husaidia kuboresha muonekano wako.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment