Wednesday, March 7, 2012
Anna Abdalla akerwa na wanaobeza viti maalum
Kuelekea siku ya wanawake duniani
Mwenyekiti wa asasi ya umoja wa wanawake wanasiasa (T-WCP) Mh. Dk Anna Margareth Abdalla, akihutubia katika sherehe za siku ya wanawake zilizofanyika Buza wilayani Temeke, Kulia kwake ni Diwani viti maalum Temeke Mh. Like Gugu na kushoto kwake ni mjumbe wa sekretarieti ya T-WCP na mwisho ni Dk Deus Kibamba kutoka Jukwaa la Katiba Tanzania.
MWENYEKITI asasi ya umoja wa wanawake wanasiasa nchini (T-WCP) Mh. Dk. Anna Margareth Abdallah, ameelezea kukerwa kwake na baadhi ya wanasiasa wanaobeza nafasi za viti maalum kwa makusudi na kuzipachika majina yasiyofaa.
Mama huyo alitoa dukuduku lake katika sherehe za siku ya mwanamke zilizofanyika katika ukumbi wa Gadafi Buza wilayani Temeke chini ya asasi hiyo ya T-WCP.
Kumekuwepo na maneneo maneno juu ya hizi nafasi za upendeleo wanazopewa wanawake na makundi mengine maalum, ambayo kwa kweli ukiyasikiliza wakati mwingine yanakatisha tamaa alisema.
“Binafsi naamini kuwa viti maalum ni haki ya mwanamke, hasa ukizingatia namna yeye alivyojitoa kupigania nchi hii kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40”.
Kwa kipindi chote hicho wanaume wamekuwa mstari wa mbele katika kujpa vyeo na kusahau kabisa nafasi ya mwanamke katika jamii kama hii ya kitanzania.
Tatizo pekee ambalo linaweza kuzungumziwa ni utaratibu wa upatikani wa hivyo viti maalum. Lakini kwa kuwa sisi wenyewe tumeshalitambua, tungependa tuachiwe wenyewe. Sisi kama wanawake tutajua jinsi ya kulitatua alisema Mh. Anna Abdalah.
Wakati mwingine inakera sana kusikia watu wakiwabeza wabunge wa viti maalum kwa kuwanyima baadhi ya haki ama kuwaita majina yasiyofaa kama vile viti vya chee na Kadhalika hii inakera kwa kweli.
“Ushauri wangu kwa wanawake wote nchini watumie nafasi za viti maalum kama shule, kwa kukaa kwa muda mchache na baada ya kubobea kurudi kwa wananchi na kuwapisha wanawake wengina katika nafasi hizo” alisisitiza.
“Kwa kuwa utakuwa ushapata uelewa wa kutosha utakaporudi kwa wananchi itakuwa ni rahisi kuingia katika mchakato wa uchaguzi na hivyo kupambana na hatimaye kufanikisha kuchukua nafasi za uongozi”.
Mwenyekiti huyo aliwahimiza wanawake kujibidiisha katika shughuli za ujasiriamali ili kujiweka sawa kiuchumi jambo litakalo warahisishia katika kujiunga na michakato mbalimbali hususani ya kugombea nafasi za uongozi.
Akitoa mada katika mkutano huo Dk. Deus Kibamba kutoka Jukwaa la katiba Tanzania amewataka wanawake kuelekeza nguvu zao katika kushiriki kwenye mchakato mzima wa uandikwaji wa katiba mpya kwa kutoa maoni yao yatakayofanikishwa kupatikana kwa katiba mpya nchini.
“Shuguli ya uandishi wa katiba yetu haiwahusu wanasheria peke yao, hivyo na nyinyi wanawake mnapaswa kuelewa kuwa mna nafasi kubwa ya kushiriki katika uandikishwaji wake kupitia maeneo mbalimbali kama vile tume, bunge maalum na hata kura ya maoni” alisema.
Mratibu wa Ulingo wilaya ya Temeke Bi Paskazia Sezari ambaye ndio mwenyeji wa shughuli hiyo aliwataka wanawake kutoa sapoti kwa wanawake wenzao watakaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
“Msijali ni kwa nafasi gani unachotakiwa kuangalia ni uwezo alionao mwanamke huyo na hivyo kuwajibika kumpigia kura. Hii itasaidi kuongeza kundi la wanawake katika uongozi”.
Maadhimisho hayo yaliwakusanya wanawake zaidi ya 300 wa vyama mbalimbali kutoka wilaya ya Temeke wakiwamo viongozi wa ngazi kadhaa yanatarajiwa kufika kilele Machi 8 mwaka huu.
Baadhi ya wanawake kutoka vikundi mbalimbali vya VOCOBA wakisherehekea siku ya wanawake. Sherehe hizo zimefanyika katika ukumbi wa Gadaffi Buza wilayani Temeke jijini Dar es salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment